Watu zaidi ya 510,000 walazimika kukimbilia nchini Sudan Kusini kutokana na vita nchini Sudan
2024-01-26 08:29:52| CRI

Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayoratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema, mapigano makali yaliyotokea kati ya Jeshi la Sudan na Kikosi cha Mwitikio wa Haraka (RSF) nchini Sudan yamewalazimisha watu 516,658 kukimbilia nchini Sudan Kusini tangu katikati ya mwezi April mwaka jana.

Ofisi hiyo imesema, hali ya kibinadamu nchini Sudan Kusini imeendelea kuwa mbaya, huku ukosefu wa usalama, mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na athari za mabadiliko ya tabianchi zikiathiri usalama wa chakula na lishe kwa familia nyingi.

Mapigano makali yamekuwa yakiendelea nchini Sudan kati ya Jeshi la nchi hiyo na kikosi cha RSF tangu katikati ya mwezi April mwaka jana, na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 9,000, wengine milioni 6 wakiwa wakimbizi wa ndani na nje ya Sudan, na wengine milioni 25 wakihitaji misaada zaidi ya kibinadamu.