Uzalishaji wa maziwa nchini Rwanda kwa mwaka wazidi tani milioni moja
2024-01-26 10:20:06| cri

Ripoti iliyotolewa na wizara ya kilimo ya Rwanda inasema uzalishaji wa maziwa nchini Rwanda kwa mwaka jana ulifikia zaidi ya tani milioni moja (lita bilioni moja), ikiwa ni uboreshaji mkubwa katika sekta ya maziwa.

Hii ina maana kuwa Rwanda ilipiga hatua kufikia lengo la zaidi ya tani milioni 1.2 katika mwaka wa fedha wa 2023/24. Uzalishaji wa maziwa umekuwa ukiongezeka kwa kasi kutoka zaidi ya tani 121,400 mwaka 2005, hadi zaidi ya tani 372,600 mwaka 2010, na tani 891,326 mwaka 2020.

Ofisa mwandamizi katika Bodi ya Maendeleo ya Kilimo ya Rwanda (RAB), Solange Uwituze amesema vichocheo vikuu vya uzalishaji wa maziwa ni pamoja na tabia ya ufugaji sifuri, kulima na kuhifadhi malisho, uvunaji na uhifadhi wa maji kwa ajili ya mifugo, bima ya mifugo na ufugaji bora wa ng'ombe wa maziwa.