Uchumi wa Afrika unatarajiwa kukua kwa asilimia 3.5 mwaka 2024
2024-01-26 08:29:07| CRI

Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Uchumi Duniani na Matarajio kwa mwaka 2024 imesema, ukuaji wa uchumi wa Afrika unaendelea kwa taratibu kwa mwaka huu kutokana na mivutano ya siasa za kijiografia, mgogoro wa hali ya hewa na hatari ya madeni.

Katika ripoti hiyo iliyozinduliwa jana mjini Addis Ababa, Ethiopia, Ofisa wa Masuala ya Uchumi wa Tume ya Uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa (UNECA) Hopestone Chavula amesema, ukuaji wa uchumi wa Afrika kwa mwaka huu utaongezeka kutoka asilimia 3.3 hadi asilimia 3.5. Amesema nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na shinikizo la kuongezeka kwa gharama za maisha kwa mwaka 2023, hususan kutokana na bei kubwa ya mafuta na chakula.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, sarafu za nchi nyingi za Afrika zimekabiliwa na shinikizo la kushuka kwa thamani yake kutokana na mapato hafifu ya kigeni na uhaba wa upatikanaji wa fedha za kigeni.