Takriban watu 42 wameuawa katika mapambano mapya kati ya jamii karibu na Sudan Kusini
2024-01-29 08:42:08| CRI

Takriban watu 42 wameuawa akiwemo mlinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa wakati wa mapambano yalipotokea katika eneo la Abyei, kati ya vijana wenye silaha wa jamii ya Twic wa jimbo la Warrap na wale wa Ngok Dinka wa jimbo la Abyei.

Ofisa wa eneo maalum la utawala la Abyei Bw. Rou Manyiel Rou, amesema mashambulizi katika maeneo ya Nyinkuac, Majbong, na Khadian yalifanywa na vijana wenye silaha kutoka jamii ya Twic kwa ushirikiano na vijana wa Nuer, wanaomtii kiongozi wao wa kiroho Gai Machiek, mashambulizi hayo yamesababisha watu 35 kujeruhiwa.

Tarehe 18 Januari Rais Salva Kiir alitoa agizo kuvitaka vikosi vya usalama kumfukuza kutoka jimbo la Warrap kiongozi wa kiroho wa Nuer Gai Machiek na vijana wanaomtii wa Nuer, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutatua mgogoro kati ya jamii za Ngok Dinka na Twic. Agizo hilo pia limevitaka vikosi vya usalama kuwakamata wanasiasa wa jamii hizo wanaochochewa mgogoro.