Takwimu mpya zinaonesha kuwa Kenya imepoteza mauzo ya nje ya thamani ya dola milioni 200 kwenda Uganda, soko lake kubwa zaidi la kikanda, tangu Oktoba 2023.
Wataalam wanaonya kuwa itapoteza zaidi katika siku zijazo, wakati vita juu ya uagizaji wa mafuta ya petroli kutoka nje vinaongezeka, huku miundombinu mikuu ya mafuta ikiwa katika hatari ya kutumiwa kwa kiwango cha chini sana.
Wiki iliyopita, Uganda ilitangaza kuhamia Tanzania katika masuala ya kuagiza mafuta baada ya harakati zake za kutaka kuwa na soko lake la taifa la mafuta, “Uganda National Oil Company (Unoc)”, lisajiliwe nchini Kenya kugonga ukuta ili kurahisisha uagizaji bidhaa kupitia bandari ya Mombasa.
Waziri wa Nishati wa Uganda Ruth Nankabirwa aliwaambia waandishi wa habari mjini Kampala kwamba Kenya kuendelea kukatisha tamaa mkataba wa Unoc kunatishia uthabiti wa usambazaji wa mafuta nchini Uganda.