Watu 16 wamethibitishwa kufariki katika ajali ya boti mashariki mwa Rwanda
2024-01-29 08:43:11| CRI

Watu 16 wamethibitishwa kufariki dunia baada ya mashua kupinduka mtoni mashariki mwa Rwanda, katika ajali iliyotokea Ijumaa jioni kwenye Mto Mugesera wilayani Rwamagana.

Boti hiyo ilikumbwa na upepo mkali ikiwa imebeba abiria, hasa wakulima waliokuwa wakitoka kuvuna wilayani Ngoma, wakielekea wilayani Rwamagana, maofisa wa eneo hilo wamesema boti hiyo ilipinduka na kuzama.

Meya wa Wilaya ya Rwamagana Bw. Radjab Mbonyumuvunyi amesema hadi kufikia Jumamosi jioni, miili 14 ilikuwa imepatikana, na mingine miwili ilikuwa haijulikani ilipo.

Boti ilikuwa na jumla ya abiria 47, na 31 kati yao waliokolewa kutoka kwenye boti hiyo ambayo pia ilikuwa imepakia mazao ya kilimo yakiwemo mahindi na maharage.