Viongozi wa Afrika watoa wito wa kuharakisha maendeleo ya viwanda ili kutimiza ustawi
2024-01-29 08:29:42| CRI

Mazungumzo kuhusu Ustawi wa Afrika yaliyodumu kwa siku tatu yalifungwa Januari 27 nchini Ghana, ambapo viongozi wa Afrika walioshiriki wametoa wito kwa nchi za Afrika kushikamana na kushirikiana katika kupiga jeki maendeleo ya viwanda barani Afrika ili kutimiza ustawi.

Kwenye mazungumzo hayo, Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo amesema nchi za Afrika zinahitaji kujenga miundombinu yenye ufanisi ya uchukuzi na ugavi, kurahisisha biashara, kueneza matumizi ya teknolojia za dijitali kwenye miamala ya kimataifa, na kuchochea biashara kati ya nchi za Afrika. Amesema, utekelezaji wa sasa wa Eneo la Biashara Huria la Afrika (AfCFTA) umetoa fursa nyingi zaidi kwa biashara za kuvuka mpaka, na unatarajiwa kuchangia ukuaji wa uchumi na kulijenga bara la Afrika lenye mafungamano zaidi.

Mazungumzo hayo yaliyoandaliwa kwa pamoja na taasisi mbalimbali ikiwemo Sekritarieti ya AfCFTA, yanalenga kuweka jukwaa la mawasiliano kwa wanasiasa na wafanyabiashara wa Afrika, kwa lengo la kutafuta njia ya kutimiza ustawi wa Afrika.