China yaitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai iheshimu mamlaka ya mahakama ya Sudan
2024-01-30 09:03:14| CRI

Naibu mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Balozi Dai Bing, jana kwenye mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu masuala ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai dhidi ya Sudan, ameitaka Mahakama hiyo iendelee kufuata kanuni za Mkataba wa Roma, kushikilia msimamo wa haki na bila upendeleo, kuheshimu mamlaka ya mahakama ya Sudan pamoja na maoni yake halali.

Balozi huyu ameeleza kuwa kurejesha utaratibu wa kijamii nchini Sudan ni msingi wa kuhakikisha utekelezaji sheria wa haki. Mahakama ya Kimataifa ya Jinai inapaswa kuzingatia hali ya amani na utulivu nchini Sudan na kuchukua jukumu la kiujenzi katika kutatua mgogoro wa Sudan kwa njia inayofaa.

Amesema China inaunga mkono hatua ya kuadhibu uhalifu mkubwa ili kulinda amani na usalama wa kimataifa, na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai lazima itumie mamlaka yake kwa mujibu wa sheria na kwa usawa, na kuepuka kuegemea upande wa kisiasa na kutumia vigezo viwili, ili kulinda kihalisi haki na usawa kwenye masuala ya kimataifa.