Ethiopia yazindua ujenzi wa kampuni ya ndani ya kutengeneza chanjo
2024-01-31 08:33:39| CRI

Vyombo vya habari vya Ethiopia vimeripoti kuwa serikali ya Ethiopia imezindua ujenzi wa kampuni ya kutengeneza chanjo, ShieldVax Enterprise, ili kuchochea uzalishaji wa chanjo kwa matumizi ya ndani na nje ya nchi.

Shirika la habari la Ethiopia Fana, limesema kampuni ya kutengeneza chanjo yenye uwekezaji wa zaidi ya dola milioni 70 za Kimarekani, itajengwa ndani ya eneo la Hifadhi ya Viwanda la Kilinto lililojengwa na wachina nchini Ethiopia, nje kidogo ya mji wa Addis Ababa.

Wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda hicho, Waziri wa Afya wa Ethiopia Bw. Lia Tadesse amesema ujenzi huo ni ushahidi wa juhudi zinazoendelea za serikali ya Ethiopia katika kuhakikisha afya kwa wote.

Amesema janga la COVID-19 lilionesha umuhimu wa miundombinu thabiti ya huduma za afya na uwezo wa kutengeneza chanjo, na kusisitiza kuwa mradi huo unatarajiwa kuleta uboreshwaji mkubwa katika usambazaji wa chanjo kwa matumizi ya nyumbani na nchi jirani.