IMF yapandisha makadirio ya ukuaji wa uchumi wa dunia kwa mwaka huu
2024-01-31 08:54:44| CRI

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limesema uchumi wa dunia kwa mwaka huu unatarajiwa kukua hadi asilimia 3.1, ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.2 ikilinganishwa na makadirio  ya Oktoba mwaka jana.

Kwenye ripoti iliyotolewa jana IMF imesema takwimu hizo zinaonyesha kuwa makadirio ya ukuaji wa uchumi wa China, Marekani na baadhi ya masoko makubwa yanayoibukia pamoja na nchi nyingine zinazoendelea yameongezeka, ambapo ongezeko la uchumi kwa nchi zilizoendelea linatabiriwa kufikia asilimia 1.5 huku ukuaji wa uchumi kwa nchi zinazoendelea na masoko yanayoibukia ukitarajiwa kufikia asilimia 4.1.

Ripoti pia imeeleza kuwa mfumuko wa bei unapungua kwa kasi zaidi katika maeneo mengi duniani kuliko ilivyotarajiwa, lakini mchumi mkuu wa IMF Pierre-Olivier Gourinchas ameonya kuwa bado unakabiliwa na hatari ya kupanda wakati bidhaa kuu na minyororo ya usambazaji ikiathiriwa na kuongezeka kwa mvutano wa siasa za kijiografia katika eneo la Mashariki ya Kati na Bahari ya Sham.