UM yazindua mpango wa kibinadamu kwa Somalia
2024-01-31 08:39:47| Cri

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric, amesema Umoja huo umezindua mpango wa mwaka 2024 wa mahitaji na mwitikio wa kibinadamu nchini Somalia, unaohitaji dola bilioni 1.6 za Kimarekani ili kuwasaidia watu milioni 5.2 nchini humo.

Msemaji huyo amesema mwaka jana Somalia ilikumbwa na majanga mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ukame mkali, mvua kubwa na mafuriko makubwa ambavyo havikutokea kabla, na kusababisha watu kukimbia makazi yao. Mbali na hayo, mamilioni ya watu waliendelea kukabiliwa na njaa na utapiamlo.

Amesema Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imeonya kuwa zaidi ya watu milioni 4, ambao ni karibu robo ya watu wanaoishi nchini humo, wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.