Madaktari wa China wa Nyurolojia wawasili Dar es Salaam kwa Mpango wa mwaka mmoja
2024-01-31 23:21:14| cri

Jumla ya madaktari 11 wa magonjwa ya mishipa ya fahamu kutoka China wamewasili nchini Tanzania tayari kwa ajili ya kutoa huduma ya mwaka mmoja katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Jumanne, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa MOI, Dk. Lemeri Mchome alisisitiza kuwa ujio wa madaktari hao unatoa fursa muhimu kwa wataalamu wa nchini humo kujifunza kutoka kwa wenzao wa China.

Mpango huu ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China.

"Wenzetu wa China wamepiga hatua kubwa katika matibabu ya mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu... Ninaamini kwamba hadi watakapoondoka, tutakuwa tumeboresha sana uwezo wetu," alisema Dk. Mchome.

Mbali na MOI, wataalamu hao pia watatoa huduma zao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), na Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.