Mwanamke wa Nigeria ajaribu kuendesha gari kutoka London hadi Lagos
2024-01-31 14:35:12| cri

Mtayarishaji wa maudhui ya usafiri kutoka Nigeria Pelumi Nubi ameanza jaribio la kuendesha gari kutoka London hadi Lagos, safari ya zaidi ya kilomita 7,000 (maili 4,340).

Kutoka Uingereza, Bi Nubi atavuka hadi Ufaransa na Hispania, kabla ya kuingia Afrika kupitia Morocco.

“Baada ya hapo, nitapitia jangwa la Sahara Magharibi, Mauritania, Senegal, Gambia, Guinea-Bissau, Guinea, Sierra Leone, Liberia, Mali, Burkina Faso, Ivory Coast, Ghana, Togo, Benin, na hatimaye Nigeria na kufikia Lagos, ” Bi Nubi alisema kuhusu njia yake ya kusafiri.

Ingawa changamoto kama hizo za kuendesha gari zimefanywa kwenye njia ya London hadi Lagos hapo awali, Bi Nubi alisema anaamini kuwa yeye ni mwanamke wa kwanza mweusi kujaribu safari hiyo.

"Lakini jamani, hii haihusiani na kuvunja rekodi. Ni kuhusu kuionesha dunia kuwa ‘haiwezekani’ ni neno tu,” alisema alipotangaza changamoto hiyo kwa mara ya kwanza Novemba mwaka jana.

Wiki iliyopita, Bi Nubi alisema kwamba safari hiyo imechukua mwaka mmoja kupanga na kuweka akiba ya fedha.

Msafiri mwenye bidii, Bi Nubi ametembelea nchi 80. Mara nyingi anaonesha ushujaa wake wa kusafiri kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.