Mwanamke Amchoma Jirani kwa Mafuta ya Kupikia Kisa Kuiga Mtindo Aliokuwa Amesuka
2024-01-31 14:35:40| cri

Mwanamke mmoja nchini Kenya anakabiliwa na shtaka la kumdhuru jirani yake. Kwa mujibu wa uchunguzi wa polisi, Catherine Wanjiru ambaye ni mshukiwa anadaiwa kumsababishia majeraha mabaya usoni Sherry Nyanchomba kwa kummiminia mafuta ya kupikia yaliyokuwa yakichemka.

Januari 16, Nyanchomba alikutana na Wanjiru kwenye lango la makazi yao Dandora mishale ya saa sita usiku. Mshukiwa huyo, alipoona wamefanana mtindo wao wa nywele, alimshutumu Nyanchomba kwa kumuiga.

Wawili hao, walikuwa na nywele fupi zenye rangi sawa. Mshitakiwa huyo inasemekana alikwenda kwenye stendi ya muuza samaki iliyokuwa jirani na eneo hilo, ambapo inadaiwa alikamata kijiko cha kukaangia na kummwagia Nyanchomba mafuta ya moto usoni. Hali hii iliongezeka na kuwa ugomvi wa kuingiana mwilini, na kusababisha meno ya Nyanchomba kung'olewa huku Wanjiru akishikilia taya yake kwa nguvu. Nyanchomba alipatiwa matibabu katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki huko Embakasi kabla ya suala hilo kuripotiwa polisi.