Serikali ya Tanzania yasema tathmini ya nchi nzima kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi inaendelea
2024-02-01 23:07:45| cri

Serikali ya Tanzania imesema timu ya wataalamu wa Ofisi ya Rais (Muungano na Mazingira) kwa kushirikiana na Idara za kisekta wameanza tathmini ya athari za mabadiliko ya tabianchi nchi nzima.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo ameliambia Bunge jana Jumatano wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mtambwe (ACT), Khalifa Mohamed Issa. Mbunge huyo alisema visiwa vya Unguja na Pemba vimeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na kusababisha baadhi ya makazi ya watu kuzama majini.

Katika swali lake mbunge huyo alisema kuwa visiwa hivyo vimeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na kusababisha baadhi ya maeneo kuzama. Alitaka kujua ni lini serikali itafanya utafiti na kuja na hatua gani fupi na ndefu za kukabiliana na hali hiyo.

Akijibu Dk Jafo alisema serikali imeanza ujenzi wa ukuta katika eneo hilo na kuongeza kuwa timu ya wataalamu kwa kushirikiana na idara za kisekta imetumwa kufanya tathmini nchi nzima.