Rais Dk.Mwinyi Aagana na Balozi Mdogo Wa China
2024-02-01 14:08:26| cri

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amekutana na Balozi mdogo wa China Mhe. Zhang Zhisheng anayefanyia kazi zake Zanzibar, na kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi nchini humo Januari 29, 2024, Ikulu Zanzibar.

Aidha Rais Dk.Mwinyi amemshukuru Balozi Mhe.Zhang Zhisheng kwa kudumisha na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Zanzibar na China katika miaka mitatu ya utumishi wake nchini, pia kwa kuratibu vyema ziara yake mwaka jana China.

Vilevile Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa China imeendelea kusaidia Zanzibar na kushirikiana katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo sekta ya afya kwa kuleta madaktari kutoka China, ufadhili wa masomo, kujengea uwezo, biashara, utalii, pamoja na kuwepo kwa kampuni za China katika kazi za miradi mbalimbali ya miundombinu ya barabara, bandari, na uwanja wa ndege.

Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi amewakaribisha wawekezaji kutoka China kwenye sekta ya utalii kujenga hoteli kwa kuongeza watalii zaidi wa China kuitembelea Zanzibar. Rais Dk. Mwinyi amesema Zanzibar itaendelea kushirikiana na kudumisha uhusiano na China ambao umetimiza miaka 60.

Naye Balozi Mhe Zhang Zhisheng amesema China itaendelea kushirikiana na Zanzibar kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia.