China na Marekani zaanza tena mazungumzo kuhusu fentanyl, kuonyesha mazungumzo ndio njia ya kutoka
2024-02-01 09:09:15| CRI

China na Marekani zimerejesha mazungumzo mjini Beijing kuhusu kusitisha utengenezaji wa viambato vya dawa ya fentanyl. 

Kwenye ufunguzi wa mazungumzo hayo mjumbe wa taifa wa China na waziri wa usalama wa Umma Bw. Wang Xiaohong alikutana na Naibu Msaidizi wa Rais wa Marekani na naibu mshauri wa Usalama wa Ndani Jen Daskal na ujumbe wa timu ya Marekani wa kukabiliana na dawa za kulevya, na pande hizo mbili zilitangaza kuanzishwa kwa kikosi kazi cha kupambana na dawa za kulevya kati ya China na Marekani.

Kuanza kwa mazungumzo hayo ni mabadiliko makubwa katika mtazamo wa Marekani kuhusu suala hilo, ikionyesha kwamba mazungumzo na ushirikiano ndio njia nzuri kwa nchi hizo mbili kutatua changamoto zilizopo kuhusu suala hilo.

Maofisa wa ngazi ya juu wa Marekani kutoka Wizara ya mambo ya nje, wizara ya fedha, Idara ya Usalama wa ndani na Idara ya na idara ya sheria wameshiriki kwenye mazungumzo hayo.

Mwezi Mei waka 2019, China iliweka dawa zote zenye Fentanyl kwenye orodha ya dawa za kulevya zinazodhibitiwa na serikali, ikimaanisha kuwa China itadhibiti dawa za Fentanyl kwa hatua kali zaidi.

Ikiwa nchi iliyoathiriwa na inayoathiriwa na dawa za kulevya, China siku zote inatekeleza sera kali ya kupiga marafuku dawa hizo. Hatua mpya dhidi ya dawa za Fentanyl inaonesha kuwa China inabeba majukumu yake katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya za aina zote.

Fentanyl ni dawa za kupunguza maumivu zenye nguvu kubwa. Katika miaka ya hivi karibuni wahalifu wa nchi kadhaa zikiwemo Marekani na Canada wanatengeneza dawa hizo na kuzifanya kuwa dawa za kulevya. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Maradhi cha Marekani, watu wengi wenye umri kati ya miaka 18 hadi 45 walifariki kutokana na kutumia dawa za kulevya za Fentanyl.

Suala la Fentanyl nchini Marekani linatokana na sababu nyingi, na serikali ya nchi hiyo inapaswa kuchukua hatua zaidi katika kupunguza matumizi ya dawa hizo.