Muhimbili yatumia saa 6 kutenganisha mapacha
2024-02-01 14:25:53| cri

Saa sita zimetumika kuwatenganisha watoto mapacha wa kike wenye umri wa miezi 10 wakazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Watoto hao ambao walizaliwa Machi mwaka jana walikuwa wameungana eneo la kifua na tumbo. Upasuaji huo ni wa kwanza kufanywa na madaktari wazawa nchini Tanzania. Akizungumza Januari 30, 2024, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Dk Rachel Mhaville amesema upasuaji huo umefanikiwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kununua vifaa tiba vya kisasa pamoja na kuwasomesha wataalamu.

Amesema, hata hivyo pamoja na kufanikiwa kufanya upasuaji huu bado wataendelea kushirikiana na wataalamu wengine kwa ajili ya kupata ujuzi zaidi na kuendeleza uhusiano.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili Dk Victor Ngota amesema upasuaji wa kuwatenganisha watoto unahitaji utaalamu wa hali ya juu hivyo ulihusisha jopo la wataalamu mbalimbali wakiwemo madaktari bingwa wa upasuaji watoto, upasuaji rekebishi, wataalamu wa usingizi, wataalamu wa lishe pamoja na wataalamu wa radiolojia.