Wananchi Rombo waomba kuua nyani
2024-02-02 23:36:31| cri

Wananchi wa kata ya Katangara Mrere, wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro wameiomba serikali kupitia wizara ya Maliasili na Utalii kuwapa kibali cha kuwaruhusu kuua nyani kwenye maeneo hayo baada ya kuwa kero kwenye makaazi yao.

Nyani hao ambao hutembea makundi kwa makundi nyakati za asubuhi na jioni wanadaiwa kuwa ni tishio katika jamii zinazoishi pembezoni mwa mto Mlembea na maeneo ya tambarare wilayani humo.

Hivi karibuni baadhi ya wanaume wilayani humo, walilivalia njuga suala la nyani hao mbele ya mbunge wao, Profesa Adolf Mkenda wakati akiwa kwenye mkutano wa hadhara kata ya Kirongo Samanga wakimwelezea kuchoka na nyani hao.