Tanzania yasitisha matumizi ya kuni magerezani
2024-02-05 23:42:14| cri

Serikali ya Tanzania imetangaza kuacha kutumia nishati ya kuni kupikia chakula katika magereza mbalimbali nchini humo, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango la utunzaji wa mazingira kwa kuacha kukata miti ili kutunza mazingira katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Kauli hiyo imetolewa wiki iliyopita na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Tanzania, Mhandisi Hamad Masauni wakati akiongoza watumishi zaidi ya mia moja kupanda miti katika eneo la Ofisi ya Wizara hiyo, Mtumba jijini Dodoma, katika zoezi ambalo pia lilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Jumanne Sagini.

Masauni amewataka watumishi kuhakikisha miti iliyopandwa na zaidi ya watumishi mia moja wa Wizara hiyo, inalindwa ili iweze kukua na kutimiza lengo la utunzaji wa mazingira.