Watalii wa China walioko ndani ya meli ya kitalii washerehekea Sikukuu ya Mwaka mpya wa jadi wa China nchini Kenya
2024-02-05 09:42:29| CRI

Kama sehemu ya sherehe za kukaribisha Sikukuu ya Mwaka mpya wa jadi wa China, watalii 200 wa China waliokuwa kwenye meli ya kifahari iliyotia nanga katika bandari ya Mombasa nchini Kenya, walitembelea vivutio vya nchi hiyo, vikiwemo Fukwe na Hifadhi za Wanyamapori.

Sikukuu ya Mwaka Mpya ya China, itaanza Februari 10, na kuashiria kwamba mwaka wa Dragon umeingia.

Mfanyabiashara wa teknolojia wa China Chu Hongge amesema kuwa amefurahi kusherehekea Mwaka Mpya wa China katika nchi ya Afrika, akipongeza upole na ukarimu wa wenyeji. Amesema hii ni mara yake ya kwanza kutembelea Afrika, na anawapenda Waafrika. Chu na wenzake walitembelea Kisiwa cha Wasini cha Kenya na Mbuga ya Taifa ya Tsavo Mashariki ili kujionea uzuri wa wanyamapori na fukwe za pwani.

Waziri wa Utalii na Wanyamapori wa Kenya Alfred Mutua ambaye pia ni miongoni mwa maafisa wakuu waliopokea meli hiyo kutoka Kampuni ya Meli ya Mediterania (MSC Poesia), amesema kuwa wanajivunia kupokea wageni wa meli hiyo ya kitalii ambao wamethibitisha kwamba Kenya bado inasalia kuwa kivutio cha utalii cha hali ya juu, akiongeza kuwa nchi hiyo ilipokea watalii 3,123 waliosafiri kwa meli ya kifahari mwaka 2023.