WHO yatoa wito wa kuchukuliwa hatua mahsusi ili kupunguza mzigo wa saratani barani Afrika
2024-02-05 09:36:31| CRI

Mzigo unaoongezeka wa saratani barani Afrika unapaswa kuchukuliwa kama mwamsho kwa serikali kuchukua hatua mahsusi ambazo zinalenga kupunguza idadi ya wagonjwa na vifo.

Hayo yamo kwenye taarifa iliyotolewa Jumapili na Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika, Matshidiso Moeti, katika Siku ya Saratani Duniani huko Nairobi nchini Kenya. Alisema bara hilo linakabiliwa na janga la saratani ambalo linaharibu maisha ya watu na kupunguza muda wa kuishi, hivyo kuna ulazima wa kuwekeza katika hatua za kuzuia na kudhibiti ugonjwa huo.

Alibainisha kuwa hali ya saratani barani Afrika inakatisha tamaa. Katika mwaka 2022, takriban wagonjwa wapya 882,000 wa saratani waligundulika katika kanda ya Afrika ya WHO na karibu vifo vya watu 573,000.

Kwa mujibu wa Moeti, takriban asilimia 50 ya saratani mpya zinazogunduliwa miongoni mwa watu wazima barani Afrika ni saratani ya matiti, shingo ya kizazi, tezi dume, utumbo mpana na ini.

Pia alipongeza maendeleo makubwa ambayo nchi za Afrika zinapata katika vita dhidi ya saratani, akibainisha kuwa nchi 17 tayari zimeanzisha vipimo vya juu vya uchunguzi kulingana na mapendekezo ya WHO.