Wahudumu wa kibinadamu watayarisha mpango wa msaada nchini Sudan ili kusaidia watu milioni 15
2024-02-06 10:42:12| CRI

Umoja wa Mataifa kwa sasa unatayarisha mpango wa kuwafikia watu milioni 15 kati ya milioni 25 wanaohitaji msaada nchini Sudan iliyokumbwa na vita.

Akiongea jana Jumatatu, Stephane Dujarric msemaji mkuu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu Martin Griffiths na Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi Filippo Grandi watashiriki katika kutangaza malengo hayo Jumatano huko Geneva.

Bw. Dujarric aliendelea kusema kwamba baada ya karibu miezi 10 ya vita, zaidi ya nusu ya watu wa Sudan, ambao ni milioni 25, wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi. Aidha vita pia vimewalazimisha zaidi ya watu milioni 1.5 kukimbilia katika mipaka ya Sudan na kuingia nchi ambazo tayari zina idadi kubwa ya wakimbizi.

Alisema Mpango huo unaoratibiwa na Umoja wa Mataifa unalenga kufikia karibu watu milioni 15 mwaka huu, wakati Mpango wa Kukabiliana na Wakimbizi wa Kikanda unalenga kusaidia karibu watu milioni 2.7 katika nchi tano jirani.