Zaidi ya watu milioni 11 wakosa makazi nchini Sudan
2024-02-06 23:08:52| cri

Sudan imesema idadi ya watu milioni 11 wamekosa makazi kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya Jeshi la nchi hiyo na Kikosi cha Mwitikio wa Haraka (RSF).

Waziri wa Habari na Utamaduni wa Sudan, Graham Abdel-Qadir amesema, kati ya watu hao, milioni 4 ni wanawake na milioni 3 ni watoto, na kuongeza kuwa, asilimia 90 ya watu hao wasio na makazi wanatokea mikoa ya Khartoum, Gezira na Darfur.

Amesisitiza ahadi ya serikali ya nchi hiyo ya kupeleka misaada ya kibinadamu kwa wahitaji kupitia mchakato na mpangilio unaohakikisha mamlaka kamili ya nchi hiyo.

Sudan imeshuhudia mapigano makali kati ya Jeshi la nchi hiyo na kikosi cha RSF yaliyoanza April 15 mwaka jana, ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, watu zaidi ya 13,000 wameuawa tangu kuanza kwa mapigano hayo.