Tanzania, AfDB zaungana kutekeleza miradi ya nishati
2024-02-06 10:32:43| cri

Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeonesha nia ya kuiunga mkono Tanzania katika miradi mbalimbali ya umeme inayofadhiliwa na Benki hiyo na miradi mingine ya nishati iliyo katika mpango wa kufadhiliwa.

Dk. Biteko ameyasema hayo jana jijini Dodoma alipokutana na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kevin Kariuki. Amesema AfDB imefadhili miradi mbalimbali ya nishati ikiwemo mradi wa umeme wa Kakono wa megawati 87.8  kwa kuchangia kiasi cha dola za Marekani milioni 161, na mradi wa Malagarasi wa megawati 49.5 kwa kuchangia kiasi cha dola milioni 120.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa AfDB, Kevin Kariuki, amesema, Benki hiyo itaendelea kufanya tathmini kuona jinsi ya kuendeleza mipango mbalimbali ya Tanzania kwenye gesi asilia, ikiwemo kupitia mpango mkakati wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ili kuainisha maeneo zaidi ya ushirikiano.