Benki kuu ya Kenya yapandisha viwango vyake hadi asilimia 13 huku kukiwa na ongezeko la mfumuko wa bei
2024-02-07 08:40:06| CRI

Benki Kuu ya Kenya (CBK) Jumanne ilipandisha kiwango chake cha mikopo hadi asilimia 13 kutoka asilimia 12.50 huku mfumuko wa bei ukiongezeka.

Katika taarifa iliyotolewa Nairobi, gavana wa CBK, Kamau Thugge, ambaye aliongoza mkutano wa Kamati ya Sera ya Fedha (MPC), alibainisha kuwa mfumuko wa bei wa jumla umeendelea kuwa juu ya kiwango kilichowekwa. Alisema kamati imeona kwamba vipengele vyote muhimu vya mfumuko wa bei yaani mafuta, chakula, na vitu visivyo chakula na visivyo mafuta (NFNF) vimeongezeka mwezi Januari.

Thugge aliongeza kuwa ongezeko la kiwango litahakikisha matarajio ya mfumuko wa bei yanaimarishwa na kushuka hadi asilimia 5.0 katikati ya kiwango kilichowekwa, pamoja na kushughulikia shinikizo lililobaki kwenye kiwango cha ubadilishaji.

Nayo Benki Kuu ya Uganda (BoU), imetangaza kwamba itadumisha kiwango cha sera yake cha asilimia 9.5, ikitaja kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei kwa ufanisi. Katika taarifa yake ya sera ya fedha ya Februari, BoU ilisema kuwa msimamo wa sera ya fedha unalingana na tathmini ya sasa ya mfumuko wa bei na matarajio ya ukuaji, ikiendelea kuunga mkono mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.