Wananchi zaidi ya 63 wakosa makazi Nachingwea, Tanzania
2024-02-07 22:57:05| cri

Zaidi ya wananchi 63 wilayani Nachingwea mkoani Lindi nchini Tanzania wamekosa makazi kufuatia mvua kubwa iliyonyesha wilayani humo na kuharibu nyumba zao huku nyingine zikiachwa na nyufa kubwa.

Wananchi hao wameiomba serikali iwasaidie wapate hifadhi salama huku walio katika mazingira ya hatari wakitakiwa kuhama mara moja kwani haijulikani mvua hizo zitamalizika lini na wako hatarini kudondokewa na nyumba mbovu zilizokosa msingi.

Mkuu wa wilaya ya Nachingwe Mohammed Moyo, ametembelea eneo la tukio na kuwapa pole waathirika wa mvua hiyo, huku akisisitiza tahadhari zaidi kwa wakazi wa eneo hilo wasiishi kwenye nyumba zao zilizobomoka kwani muda wowote zinaweza kuwadondokea.