Wachina waliopo nchini Tanzania washerehekea Sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China
2024-02-07 08:39:31| CRI

Wachina waliopo nchini Tanzania wamesherehekea Sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China kwenye tafrija iliyofanyika Jumatatu usiku katika Ubalozi wa China uliopo jijini Dar es Salaam.

Kwenye tafrija hiyo Watanzania waalikwa walijumuika na marafiki zao wa China, jambo lililodhihirisha urafiki wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.

Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, alisema Mwaka Mpya wa jadi wa China, sikukuu ambayo ni muhimu inayounganisha familia, ni kumbukumbu ya kawaida ya Wachina ndani na nje ya nchi na ni sehemu muhimu ya utamaduni wa jadi wa China. Aidha amesema inabeba amani, urafiki, maelewano na dhana nyingine za ustaarabu wa China, pamoja na matarajio ya kawaida ya binadamu wote kuunganishwa, kufurahia, kuridhika na kuwa na ustawi.

Naye Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Tanzania, Anna Makakala, aliishukuru serikali ya China kwa kuisaidia Tanzania katika kujenga uwezo wa huduma za uhamiaji na kutoa msaada wa kiteknolojia ili kuwezesha huduma za uhamiaji kufikia viwango vinavyotakiwa.

Tafrija hiyo pia ilihudhuriwa na wanadiplomasia kutoka nchi mbalimbali, viongozi wakuu wa serikali na wanataaluma.