Kiongozi wa Houthi nchini Yemen aapa kuongeza mashambulizi kama mzozo wa Gaza utaendelea
2024-02-07 08:37:56| CRI

Kundi la Houthi nchini Yemen limeapa kuongeza mashambulizi katika Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden kama mzozo wa Gaza utaendelea.

Hayo yamo kwenye hotuba iliyotolewa Jumanne na kiongozi wa kundi hilo Abdul Malik al-Houthi kwenye kituo cha televisheni cha kundi hilo al-Masirah. Amesema amezionya nchi za Marekani, Uingereza na Israel kwamba lazima waache uchokozi wao na kuacha kuzingira kwenye ukanda wa Gaza, la sivyo kundi hilo litaongeza mashambulizi zaidi.

Alitoa hotuba hiyo ili kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 20 tangu kuuawa kwa kaka yake mkubwa, Hussein Badreddin al-Houthi, ambaye ni mwanzilishi wa kundi hilo lenye silaha, na aliuawa wakati wa mapigano na jeshi la serikali ya Yemen mwaka 2004 katika ngome ya Houthi kaskazini mwa mkoa wa Saada.

Mapema siku hiyo, kundi hilo lilidai kuhusika na mashambulizi dhidi ya meli ya jeshi la majini la Marekani na meli ya biashara ya Uingereza katika Bahari ya Shamu. Al-Houthi amebainisha kuwa kundi hilo liko tayari kuvuruga usafirishaji wa meli za kimataifa.