Wakenya wengi waona hali ya kifedha itaboreka katika miezi 6 ijayo
2024-02-08 09:55:46| CRI

Robo tatu ya Wakenya wana matumaini kwamba hali yao ya kifedha itaboreka katika miezi sita ijayo.

Hayo yamesemwa na wataalam wa uchumi kwenye ripoti mpya iliyotolewa Jumatano mjini Nairobi. Kwa mujibu wa wataalam wa shirika la Old Mutual Financial Services Monitor (OMFSM) kumiliki au kuendesha biashara ndogo ndogo ni wazo kuu katika akili za Wakenya wengi.

Afisa mkuu mtendaji wa shirika la OMFSM Afrika Mashariki Arthur Oginga amesema kwenye uzinduzi wa ripoti hiyo kuwa kuna matumaini fulani miongoni mwa Wakenya licha ya mazingira magumu ya sasa.

Oginga amesema kwa sasa ni asilimia 26 pekee ya Wakenya wanaoweka akiba kwa ajili ya maisha baada ya kustaafu, wakitumai watoto wao watatoa usaidizi watakapofika uzeeni.

Ripoti hiyo inayotoa maelezo ya kina kuhusu hali ya kifedha ya Kenya, ni chapisho la kila mwaka ambalo hutolewa na Old Mutual ambayo ni kampuni ya huduma za kifedha ya Afrika inayofanya kazi katika nchi 13 za Afrika na nchini China.