Mkuu wa UM anayeshughulikia operesheni za kulinda amani awataka waasi wa M23 kusitisha mapigano mashariki mwa DR Congo
2024-02-08 09:18:25| CRI

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Operesheni za Amani Jean-Pierre Lacroix ametoa wito kwa waasi wa M23 kusitisha uhasama mara moja mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Aliyasema hayo wakati wa mkutano na wanahabari kufuatia safari yake iliyoanzia Februari 2 hadi 5 katika miji ya Goma, Beni na Bukavu, mashariki mwa nchi hiyo, ambako hali ya usalama bado ni ya wasiwasi kutokana na uhasama kati ya jeshi la Kongo na makundi yenye silaha likiwemo la M23.

Kwenye safari hiyo, Lacroix alijadili kwa kina changamoto za kiusalama na askari wake, maendeleo ya kujiondoa taratibu kwa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa nchini DRC MONUSCO na kuzuia udhalilishaji na unyanyasaji wa kingono.

Wakati wa mkutano wake na Jenerali Dyakopu Monwabisi, kamanda wa kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) nchini DRC, Lacroix alisisitiza umuhimu wa uratibu wa pamoja wa kusaidia jeshi la DRC katika mapambano yao dhidi ya makundi yenye silaha mashariki mwa DRC.