Misri kuandaa duru mpya ya mazungumzo kuhusu kusitisha mapigano Gaza huku Netanyahu akikataa pendekezo la Hamas
2024-02-08 09:50:30| CRI

Kwa mujibu wa televisheni ya al-Qahera ya Misri, duru mpya ya mazungumzo kuhusu usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza inatarajiwa kuanza leo mjini Cairo, Misri, yakiwa na lengo la kuleta utulivu katika Ukanda huo na kuachiliwa huru kwa wafungwa wa Palestina na Israel.

Misri imezitaka pande zote kuonyesha unyumbufu unaohitajika ili kufikia utulivu katika ukanda huo unaosumbuliwa na vita.

Misri na Qatar ambazo ni wafadhili wa mazungumzo hayo zimetangaza kwamba zimepokea jibu la kundi la wapiganaji wa Hamas kuhusu pendekezo la kusitisha mapigano Gaza lililoamuliwa wakati wa mkutano uliofanyika hivi karibuni nchini Ufaransa.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekataa pendekezo la Hamas la kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza siku ya Jumatano. Amewaambia waandishi wa habari kuwa "kuingia katika matakwa ya hadaa ya Hamas kutasababisha mauaji mengine.”

Matamshi haya ya Netanyahu yamekuja saa chache baada ya kundi la Hamas linaloendesha shughuli zake katika ukanda wa Gaza, kuwasilisha masharti mengi ili kujibu pendekezo la kusitisha mapigano lililosimamiwa na Qatar.