Vijana ni tegemeo kubwa la maendeleo ya nchi katika miaka ijayo. Hata hivyo, vijana wa kiume na wa kike hukabiliwa na changamoto nyingi katika ukuaji na kupevuka kwao kutoka ujana hadi utu uzima hasa katika uhusiano wa kijamii, afya na uchumi. Wakiwa ni nguvu kazi ya taifa, hivyo ili nguvu kazi hiyo izae matunda ni lazima iwe yenye uwezo na utimamu wa akili na afya kwani ndiyo vigezo muhimu vinavyomwezesha mtu yeyote kufikia adhima ya uzalishaji mali ngazi ya familia na taifa kwa ujumla.
Mbali na umuhimu wake, bado kumekuwepo na changamoto kubwa kwa vijana juu ya ufahamu wa elimu ya afya ya akili, afya ya mwili na hata afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwa vijana hasa wasichana, hali inayohatarisha mstakabali wa vijana wengi kutokana na kuathirika afya ya mwili pale wanapopata magonjwa mbalimbali.
Kwa kuliona hilo serikali za nchi mbalimbali za Afrika kupitia Wizara zake za Afya, ama wadau mbalimbali wa maendeleo zimeendelea kutoa elimu kwa vijana wa makundi tofauti ndani ya jamii ili kujua namna ya kutunza afya zao popote pale wanapokuwepo. Kundi la vijana limeonekana kuwekewa mkazo zaidi kwani linatajwa kuathiriwa zaidi na changamoto zitokanazo na kutozingatia elimu ya afya kwa ujumla kwani hata kwa upande wa janga la ukimwi takwimu zinaonesha kuwa asilimia kubwa ya watu wote wanaoishi na virusi vya ukimwi ni hawahawa vijana. Hivyo basi leo kwenye kipindi cha ukumbi wa wanawake tutaangalia Changamoto mbalimbali za afya kwa vijana.