Waziri Mkuu wa Tanzania aagiza kufanywa tathmini na ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea
2024-02-09 08:46:55| cri

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameagiza mamlaka husika kutathmini na kukarabati miundombinu, ikiwemo barabara na madaraja, yaliyoharibiwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini kote.

Akijibu maswali bungeni Alhamisi mjini Dodoma, Majaliwa aliwaagiza Wakala wa Barabara wa Tanzania(TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kufanya tathmini na ukarabati huo kote nchini, akisema serikali inachukua hatua za kuhakikisha miundombinu iliyoharibiwa na mvua inarejeshwa ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi,

Wakati huo huo, Majaliwa amewataka wananchi wanaoishi kando ya mabonde kuhama na kuhamia maeneo ya miinuko kwa sababu mvua bado zinaendelea kunyesha na kusababisha madhara makubwa.

Mvua zinazonyesha hivi sasa zimesababisha vifo vya watu wengi na kuwaacha maelfu kukosa makazi baada ya nyumba zao, mazao ya shambani, barabara na madaraja katika maeneo tofauti nchini kuharibiwa.