Tamasha kubwa la “Chunwan” lakaribisha mwaka mpya wa jadi wa China wa Dragon
2024-02-09 20:14:06| cri

Leo tarehe 9 Februari ni mkesha wa mwaka mpya wa jadi wa China wa Dragon. Saa 2 usiku, likiambatanishwa na wimbo na ngoma, tamasha la mkesha wa mwaka mpya wa jadi wa China ambalo limeandaliwa na Shirika kuu la utangazaji la China CMG limerushwa hewani.

Wakati huu, mamia ya mamilioni ya watazamaji kote duniani wanaketi mbele ya televisheni au kupitia new media, kutazama tamasha hilo moja kwa moja kwa pamoja.

Mwaka 1983, kituo cha taifa cha televisheni cha China CCTV kiliandaa tamasha la kwanza la sanaa na utamaduni la mwaka mpya wa jadi wa China , liitwalo “Chunwan”. Kila ifikapo mkesha wa mwaka mpya wa jadi wa China, wanafamilia kukusanyika kukaa pamoja kutazama tamasha hilo imekuwa ni desturi ya watu wa China.

Tamasha hilo la mwaka 2024 limejumuisha utamaduni wa jadi wa China, likitumia njia za sanaa za kisasa na uvumbuzi wa teknolojia mbalimbali za mwanga na kivuli, linajumuisha maonesho ya nyimbo na ngoma, mazingaombwe, opera, wushu, sarakasi na vipindi vya aina mbalimbali. Mbali na watu wa China, watu kutoka miji 90 ya nchi 49 duniani pia wanaweza kutazama tamasha hilo moja kwa moja kupitia luninga zaidi ya 3000 zilizofungwa nje ya nyumba.