Maonesho ya Miaohui ya kuadhimisha Mwaka Mpya wa Jadi wa Kichina yafanyika nchini Uganda
2024-02-09 10:24:26| Cri

Maonesho ya Miaohui ya kuadhimisha Mwaka Mpya wa Jadi wa Kichina yaliyoandaliwa na Ubalozi wa China nchini Uganda pamoja na idara ya utamaduni ya Uganda yamefanyika hivi karibuni mjini Kampala, na kuwavutia maelfu ya watu waliotaka kushuhudia utamaduni maalumu wa Kichina. 

Maelfu ya Waganda na Wachina wanaoishi nchini Uganda walikusanyika katika Uwanja wa Uhuru ulioko eneo la Kololo mjini Kampala kwa ajili ya maonyesho hayo, ambayo ni maandalizi ya kukaribisha tamasha la Spring, ambalo litaanzia tarehe 10 hadi tarehe 16 Februari mwaka huu. Baadhi ya Waganda walihudhuria hafla hiyo wakiwa wamevalia mavazi ya kitamaduni ya Kichina, hivyo kuimarisha zaidi mseto wa kitamaduni.

Zaidi ya hayo, katika ishara ya upendo wa dhati na kwa ajili ya kutoa misaada, wasanii wa uchoraji picha wa Uganda na China waliungana, na kuchora pamoja ili kuunda kazi nzuri ya sanaa, inayoashiria moyo wa ushirikiano na umoja kati ya nchi hizo mbili.

"Watu wanatazama Mashariki, na jua linapochomoza, mambo mengi mazuri yatatokea, kwa hiyo inamaanisha kuwa maisha yetu ya baadaye ni mazuri. Na inaitwa 'ishara Nyekundu katika eneo la Mashariki,' hali ambayo pia inaashiria matumaini. Napenda nyakati za mchana na jioni. Unapotazama angani, mambo yote mazuri yanaweza kukutia moyo. Una hisia nzuri kuhusu maisha yako ya baadaye, "alisema Lin Yaqun, msanii wa picha wa China.

Bruno Ruganzu, mchora picha wa Uganda, alisisitiza umuhimu wa shughuli za kisanii, kama vile uchoraji na maonyesho ya kitamaduni, kama njia muhimu za kukuza uelewa na maelewano kati ya jamii mbalimbali kote duniani.

"Siku zote napenda kufanya ushirikiano na wasanii wengine kama msanii kwa sababu sanaa ni lugha ya watu wote, kiukweli tunapozungumzia sanaa basi hakuna mipaka, hakuna nchi, hakuna rangi, ni njia ya kuwasiliana na kuweza kubadilishana mawazo na mazungumzo. Na China ina historia ndefu ya kuelewa ustaarabu wa watu wengine," Ruganzu alisema.

Ingawa China iko umbali wa maelfu ya maili na Afrika, lakini mawasiliano ya utamaduni kati ya pande hizo mbili yalianza mapema sana. Mwanzoni mwa karne ya 15, ofisa wa juu wa serikali ya enzi ya Ming ya China Zheng He, aliongoza meli nyingi kubwa hadi Bahari ya Magharibi mara saba, na nne kati ya hizo alifika pwani ya Afrika Mashariki. Aliwaletea Waafrika kauri na hariri nzuri za kichina, na kuchukua vitu maalumu vya kiafrika. Katika Kisiwa cha Lamu nchini Kenya, kuna hadithi kwamba baadhi ya mabaharia wa China walikaa na kuishi huko mpaka sasa.

Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na maendeleo ya kina ya majukwaa ya ushirikiano ikiwemo Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, na ujenzi wa pamoja wa pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, kuimarisha mawasiliano ya utamaduni kumezidi kuwa moja ya vipaumbele kwa pande zote mbili ili kuimarisha na kuendeleza ushirikiano wao. Kuna msemo wa Kichina unaosema, “Uhusiano mzuri kati ya nchi unategemea urafiki kati ya watu wao.” Mawasiliano ya watu na utamaduni ni muhimu katika kuendeleza na kudumisha ushirikiano kati ya China na Afrika.