Takriban watoto elfu 78 wakimbia makazi yao wiki iliyopita mashariki mwa DR Congo kutokana na migogoro
2024-02-09 08:44:54| cri

Kuongezeka kwa ghasia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kumewalazimu takriban watoto elfu 78 kukimbia makazi yao katika wiki iliyopita, huku maelfu ya watu wakielekea Goma, mji mkuu wa jimbo la mashariki la Kivu Kaskazini.

Hayo yamesemwa na shirika la hisani la kimataifa Save the Children Alhamisi kupitia taarifa yake, ambayo pia imesema mapigano mapya kati ya jeshi la taifa na kundi la waasi la M23, yamesababisha takriban watu laki 1.5 kukimbia makazi yao, zaidi ya nusu yao wakiwa watoto, tangu Februari 2, 2024. Wazazi wameripoti kuwa watoto wengi wametenganishwa na wazazi wao katika ghasia hizo, ingawa idadi ya watoto waliopotea bado haijajulikana.

Shirika hilo pia limesema matumizi ya mizinga, ndege zisizo na rubani na vilipuzi mashariki mwa DRC yanaua na kujeruhi raia na kuharibu miundombinu muhimu.

Habari nyingine zinasema takriban watu 18 walifariki Alhamisi katika ajali ya barabarani huko Kimbanseke, mtaa wa pembezoni uliopo Kinshasa, nchini DRC. Kwa mujibu wa Jeannot Canon, meya wa Kimbanseke, lori la kubeba taka lililokuwa likitoka uwanja wa ndege wa N'djili liligonga basi dogo lililokuwa likijaribu kuingia kwenye barabara kuu ya Lumumba kuelekea katikati mwa jiji.