Matokeo ya ushirikiano kati ya China na Afrika yafanya Kombe la Afrika kung'aa zaidi
2024-02-09 10:26:00| Cri

Michuano ya 34 ya Kombe la Mataifa ya Afrika inaendelea nchini Cote d'Ivoire. Kwenye lango la kuingia katika Uwanja wa Olympic wa Abidjan, mji mkuu wa kiuchumi wa Cote d'Ivoire, mashabiki kutoka nchi mbalimbali waliokuwa wamevalia bendera za nchi zao na kushikilia pembe ya kupuliza wamejaa, wakisubiri kuingia uwanjani kutazama mashindano ya soka.

Kijana mmoja kutoka Togo amesema, ametoka Lome hadi Abidjan ili kutazama Kombe la Mataifa ya Afrika. Alipotazama ligi za soka za Ulaya, alifikiria ni lini Afrika itakuwa na viwanja vizuri kama vile vya Wazungu. Lakini sasa ameuona mjini Abidjan, na kuwashukuru marafiki wa China ambao wamejenga uwanja huo.

Ukiwa ni uwanja mkuu wa mashindano ya AFCON, Uwanja wa Olimpiki wa Abidjan ni moja ya miradi muhimu kufuatia ushirikiano wa pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” kati ya China na Afrika. Uwanja huu wenye viti 60,000 ndio uwanja mkubwa zaidi, wenye vifaa na teknolojia ya juu zaidi kwenye kanda ya Afrika ya Magharibi. Wajenzi wa China na Cote d'Ivoire walifanya kazi pamoja na kuukamilisha ndani ya miaka miwili tu.

Katika miaka ya hivi karibuni, chini ya mwongozo wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, na ujenzi wa pamoja wa Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, uhusiano wa ushirikiano kati ya China na Afrika umeendelea kuimarika zaidi. China imesaidia nchi za Afrika kujenga miundombinu mingi, ikiwemo viwanja vikubwa 45 vya michezo. Nchini Côte d'Ivoire, licha ya Uwanja wa Olimpiki wa Abidjan, miongoni mwa viwanja vingine vitano vinavyotumika katika mechi za AFCON, Uwanja wa San Pedro na Uwanja wa Korhogo pia vilijengwa na makampuni ya China.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kombe la Afrika la Côte d'Ivoire Francois Albert Amachia, ameishukuru China na kusema, wanafurahia ushirikiano mzuri kati ya nchi hiyo na China, na kwamba viwanja hivyo vya michezo ni uthibitisho halisi wa urafiki huo.

Katika kijiji cha Yaou, kilichoko zaidi ya kilomita 40 mashariki mwa Abidjan, wanakijiji wameketi katika ukumbi wa kijiji hicho kutazama mashindano kati ya timu ya Côte d'Ivoire na Guinea-Bissau kupitia TV. Dakika 5 baada ya kuanza kwa mashindano hayo, timu ya Cote d'Ivoire ili pata bao la kwanza, na mashabiki wa kijiji hicho walisisimka, na kila mtu alikuwa anashangilia na kurukaruka mbele ya TV, kama kwamba walikuwa kwenye uwanja wa michezo. Wanakijiji hao wameishukuru kampuni ya StarTimes ya China kwa kukipatia kijiji hicho mawimbi ya televisheni ya satelaiti, hivyo kuwawezesha kutazama soka. Hapo awali, kama maeneo mengine ya vijijini barani Afrika, Kijiji cha Yaou kilikuwa na mawimbi ya televisheni ya analogi yenye uwezo mdogo, na mara kwa mara mawimbi hayo yalikuwa yanapotea kabisa.

Mwezi Desemba mwaka 2015, serikali ya China ilitangaza utekelezaji wa “Mipango Kumi ya Ushirikiano kati ya China na Afrika.” Miongoni mwa mipango hiyo, mradi wa “Vijiji Elfu Kumi” unalenga kutoa mawimbi ya TV ya satelaiti kwa vijiji 10,000 barani Afrika. Hadi kufikia Desemba mwaka 2023, mradi huo ulikamilisha kwa mafanikio ujenzi katika vijiji 9,512 kwenye nchi 20 za Afrika, na kuwanufaisha karibu watu milioni 10.

Kampuni ya TECNO ya China ambayo ni mfadhili rasmi wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, imetangaza kuwa, katika miaka mitano ijayo, itasaidia nchi 10 za Afrika ikiwemo Cote d'Ivoire, Nigeria, Senegal, na Kenya, kukarabati viwanja 100 vya soka, ili vijana wa Afrika waweze kucheza soka katika mazingira mazuri na yenye usalama.