Kwa nini watalii wa China waacha kutalii nchi za Magharibi?
2024-02-09 10:23:24| Cri

Hivi karibuni, Shirika la habari la Marekani Bloomberg lilitoa ripoti yenye kichwa kinachosema “China imesababisha hasara ya dola bilioni 130 za Kimarekani kwa sekta ya utalii duniani.” Ripoti hiyo inadai kuwa, ikiwa kundi kubwa zaidi la watalii duniani, watalii wa China sasa hawaonekani tena katika nchi za magharibi ambazo awali ziliwavutia zaidi, na sasa wanapenda zaidi kutalii katika nchi nyingine haswa nchi za Mashariki ya Kati. Ripoti hiyo pia imechambua sababu zilizosababisha mabadiliko hayo, ikiwa ni pamoja na mambo ya kiuchumi, mivutano ya kisiasa, na migogoro ya kikanda.

Lakini jibu la suala hilo ni wazi. Katika miaka kadhaa iliyopita, nchi za Magharibi hasa Marekani zimeichukulia China kama adui yao, mara kwa mara zimeipaka matope, kuiwekea vikwazo, na pia kuzuia mawasiliano ya watu. Hata baadhi ya vyombo vya habari vimedai watalii wa China wanaweza kuwa majasusi, vitendo ambavyo vimewachukiza sana Wachina.

Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi wa Kichina unakaribia. Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Utamaduni na Utalii ya China zinaonesha kuwa, idadi ya watu walioagiza kufanya utalii wakati wa sikukuu hiyo imeongezeka kwa mara 7 ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hiki, na kati yao asilimia 34 watatalii katika nchi za nje.

Lakini mabadiliko ni kwamba, watalii wa China hawajachagua nchi za magharibi walizopenda zamani kufanya utalii, na badala yake wamechagua kutalii katika nchi rafiki zikiwemo Thailand, Singapore, Maldives, Urusi, Falme za Kiarabu, Malaysia na Indonesia.

Bloomberg pia iliweka ripoti hiyo kwa njia ya video kwenye mtandao wa kijamii wa X, ambapo mwanamtandao mmoja amesema, labda wao (Wachina) hawafurahii kuitwa watu wanaoeneza virusi, na mwingine amesema, labda kudai kwamba China ni adui si mkakati mzuri wa kukuza utalii. Mwanahabari wa New Zealand Amber Ran amesema, nchi za magharibi zinapenda kuikosoa China, zinaiambia dunia kuwa China ni tishio, pia zinaeneza habari zisizo za kweli kwamba, Wayghur wa Xinjiang wanateseka, na wakati huo huo, zinapuuza mateso ya kweli ya Wapalestina. Sasa wanataka watalii wa China wafanye nini?

Baadhi ya wanamtandao wamekosoa vitendo vya vyombo vya habari vya Magharibi, wakisema kama vyombo vya habari ikiwemo Bloomberg havikutumia muda mwingi kupaka matope China, Wachina wangejisikia kukaribishwa zaidi katika nchi za Magharibi. Sasa wamechagua nchi nyingine zinazoonesha urafiki kwao.

Inaonekana kwamba watu duniani kote wanafahamu vizuri sababu ya kutoweka kwa watalii wa China katika nchi za Magharibi. Sasa ni wakati kwa wanasiasa wa nchi za Magharibi kutafakari madhara ya kuichukulia China kama adui.