Rwanda yatoa tahadhari ya ugonjwa wa macho mekundu
2024-02-12 09:11:00| CRI

Wizara ya Afya ya Rwanda Jumapili iliwataka wananchi kuchukua hatua za tahadhari, ikiwa ni pamoja na kunawa mikono mara kwa mara, ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa macho mekundu (Red eyes) unaoambukiza sana kufuatia kuzuka kwenye nchi za Kenya na Tanzania zilizopo kwenye kanda yao.

Wizara imesema ugonjwa huo unaenea kwa kugusa macho ya watu walioambukizwa au sehemu zilizoambukizwa. Ikitoa ushauri wake kwa umma juu ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuepuka maambukizi, wizara imewataka walioambukizwa kuepuka kwenda kwenye maeneo yenye watu wengi, kukumbatiana na kupeana mikono.

Pia imetahadharisha wale walioambukizwa kuepuka kuogelea kwenye mabwawa ya kuogelea ya umma na kutumia pamoja vifaa. Aidha wanafamilia pia wametahadharishwa kutolala kitanda kimoja na walioambukizwa ugonjwa huo. Ilishauri wale walio na dalili kali ikiwa ni pamoja na macho kuwa mekundu, kuvimba na uoni hafifu kutafuta matibabu haraka ili kuepusha hatari ya ulemavu wa macho.