Wataalamu wa Teknolojia wakutana huko Nairobi kuhimiza ujenzi wa miji ya kisasa barani Afrika
2024-02-13 09:49:54| CRI

Wataalamu wa teknolojia jana walikutana huko Nairobi, mji mkuu wa Kenya kuhimiza maendeleo ya miji ya kisasa barani Afrika.

Mkutano huo unaohusu miji inayoendeshwa na data umehudhuriwa na wadau zaidi ya 100 wakiwemo maofisa waandamizi wa serikali, sekta binafsi na wasomi kutoka Afrika, ili kukuza uvumbuzi na ushirikiano katika maendeleo ya miji ya kisasa barani humo, inayotoa huduma bora kwa wakazi wake.

Katibu mkuu wa wizara ya habari, mawasiliano na uchumi wa kidijitali Bw. Edward Kisiang’ani katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa mkutano huo amesema, Kenya hivi sasa iko mstari wa mbele katika mipango mipya ya maendeleo ya mji wa Teknolojia wa Konza, ambao ni wa kisasa zaidi ulioko umbali wa kilomita 70 kusini mwa Nairobi, inayojumuisha kanuni endelevu, za uvumbuzi na shirikishi.

Bw. Kisiang’ani amesema, awamu ya kwanza ya mji wa Konza inakaribia kukamilika, ikimaanisha hatua kubwa inayopigwa katika ahadi yao ya kujenga miji ya kisasa na thabiti zaidi.