Shilingi ya Kenya yabadilisha mwelekeo wa kushuka dhidi ya sarafu za kimataifa
2024-02-14 09:27:00| CRI

Shilingi ya Kenya imebadilisha mwelekeo wa kushuka dhidi ya sarafu kubwa duniani, ambao uliendelea kuwepo mwaka jana, na kufikia kiwango cha juu zaidi dhidi ya dola ya Marekani siku ya Jumanne.

Benki Kuu ya Kenya imeweka kuwa dola moja kwa shilingi 158.6, likiwa ni ongezeko kutoka kiwango cha chini cha shilingi 161 katika miaka 30 iliyopita. Kwa mujibu wa benki kuu Shilingi imerekodi na kudumisha ongezeko tangu Februari 8 na inatarajiwa kuongezeka zaidi katika siku zijazo.

Benki hiyo ilisema kwa upande wa pauni, Shilingi ya Kenya pia imeongeza kiwango cha mabadilishano na kuwa pauni 1 kwa shilingi 200.1, huku euro 1 ikiwa shilingi 170.8. Mbali na hapo shilingi ya Kenya pia imeongezeka dhidi ya sarafu za Afrika Mashariki, ikipanda dhidi ya shilingi za Tanzania na Uganda.

Wakati huohuo Waziri wa Hazina ya Kitaifa na Mipango ya Kiuchumi, Njuguna Ndung'u, amesema Kenya imefanikiwa kukusanya dola za Kimarekani bilioni 1.5 kwenye ununuzi wake wa dhamana za Euro ulioanza Februari 7, na kupunguza uwezekano wa kushindwa kulipa deni lake la dola bilioni 2 linalopaswa kulipwa mwezi Juni. Ununuzi huo ulifikia dola bilioni 6, ukiruhusu bei kubwa na kuongezeka kwa utoaji.