AU yalaani kuwatumia watoto katika mizozo ya kivita barani Afrika
2024-02-14 09:29:23| CRI

Umoja wa Afrika (AU) umelaani vikali uandikishaji na kuwatumia watoto katika mizozo ya kivita barani Afrika na kutaka kukomeshwa kwa vitendo hivyo.

Wito huo umetolewa katika Siku ya Kimataifa ya Kupinga Matumizi ya Askari Watoto, ambayo huadhimishwa kila mwaka Februari 12. Kauli hiyo ambayo ilitolewa na Kamishna wa AU wa masuala ya kisiasa, amani na usalama Bankole Adeoye, na mwakilishi wa kudumu wa Gambia katika Umoja wa Afrika Jainaba Jagne, ambao ni wenyeviti wenza wa Jukwaa la Afrika kuhusu Watoto walioathiriwa na Migogoro ya Silaha (APCAAC), ilitaka kufanywa juhudi za pamoja dhidi ya vitendo hivyo.

AU imehimiza nchi wanachama wake kuchukua hatua za kimfumo na zilizolengwa kulinda watoto dhidi ya ukiukwaji wa haki zao zote, haswa kuwaajiri na kuwatumia wavulana na wasichana katika mazingira ya migogoro. Imezitaka nchi za Afrika kuzidisha juhudi za kuhakikisha watoto wanaachiliwa kila inapopatikana fursa, huku watoto wakipewa kipaumbele katika mchakato wa kuwaondoa.