Kenya yasema watoto milioni 12 wameathiriwa na majanga ya hali ya hewa
2024-02-15 09:27:16| cri

Kenya ilisema Jumatano kuwa zaidi ya watoto milioni 12 nchini humo wameathiriwa na hatari zinazohusiana na majanga ya hali ya hewa na mifadhaiko.

Kwenye taarifa iliyotolewa mjini Nairobi nchini Kenya, Wizara ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu ilisema kati ya idadi hiyo, milioni 2.4 kati yao wanaishi katika kaunti kame na nusu kame ambako athari za mabadiliko ya tabianchi ni kubwa mno.

Baadhi ya madhara makubwa ya mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri watoto ni pamoja na magonjwa kama kipindupindu yanayosababishwa na mafuriko na utapiamlo kutokana na ukame. Wizara hiyo imeongeza kuwa kuna watu waliohama kwenye makazi yao kutokana na ukame na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa, ambapo matukio hayo mawili ya hali ya hewa yamekuwa ya kawaida nchini Kenya katika miaka iliyopita.