Kamati ya bunge la Uganda yataka kuangaliwa upya kwa sera ya taifa ya wakimbizi
2024-02-16 09:23:48| CRI

Kamati ya bunge nchini Uganda imehimiza kuangaliwa upya kwa sera ya taifa ya wakimbizi wakati nchi hiyo ikikabiliana na ongezeko la idadi ya wakimbizi.

Kamati hiyo ya Fursa Sawa katika ripoti yake bungeni ilisema kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi kutoka nchi jirani kunaathiri vibaya utoaji wa huduma za kijamii kama vile elimu na afya. Ripoti hiyo pia imesema kupungua kwa bajeti kutoka kwa wafadhili kumezidisha hali ambapo baadhi ya walimu wamepoteza kazi, na wakimbizi wanakabiliwa na uhaba wa chakula.

Kamati hiyo ilipendekeza bungeni kwamba sera ya nchi ya kufungua mlango ambapo wakimbizi wanaruhusiwa kuingia nchini humo bila vizuizi inahitaji kuangaliwa upya ili kudhibiti idadi. Pia ilipendekeza kuwa serikali ishirikiane na nchi nyingine na taasisi za kimataifa katika kuwahamisha wakimbizi hadi nchi za tatu.