Mwenyekiti wa Baraza la Utendaji la AU alaani mabadiliko ya serikali kinyume na katiba barani Afrika
2024-02-16 09:22:16| CRI

Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Comoro ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Utendaji la Umoja wa Afrika (AU) Dhoihir Dhoulkamal, amelaani mwenendo unaoongezeka wa mabadiliko ya serikali kinyume na katiba barani Afrika, akisema ingawa ugaidi na msimamo mkali unaendelea kutishia maisha ya baadhi ya nchi za Afrika, lakini janga la mabadiliko hayo limetikisa bara katika miaka miwili iliyopita.

Dhoulkamal ameyasema hayo alipokuwa akihutubia katika ufunguzi wa Kikao cha 44 cha Kawaida cha Baraza la Utendaji la Umoja wa Afrika kilichoanza Jumatano kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika yaliyopo Addis Ababa nchini Ethiopia. Alisema mwenendo huo unaokua katika bara zima umehatarisha maendeleo chanya yaliyopatikana katika kukuza demokrasia barani Afrika.

AU katika miaka ya hivi karibuni imethibitisha tena "kutovumilia" mabadiliko ya serikali kinyume na katiba barani Afrika, huku ikitoa wito wa kurejea haraka kwa utaratibu wa kikatiba kufuatia mapinduzi ya kijeshi nchini Gabon, Niger, Mali na Burkina Faso, miongoni mwa mengine.