Inafahamika kuwa tarehe 6 Februari ya kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji. Mwaka 2003, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha kuwa Februari 6 kila mwaka kuwa siku rasmi ya kimataifa ya kupinga ukeketaji duniani kote. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilifikia uamuzi huu baada ya kutathimini na kuona athari kubwa zitokanazo na vitendo vya ukeketaji kwa mtoto wa kike. Yapo madhara mengi yanayosababishwa na ukeketaji, ambayo yanaweza kuwa ya kiafya au hata kisaikolojia. Juhudi kubwa zimefanyika kuzisaidia jamii kuondokana na mila potofu, ikiwemo ukeketaji, kuna miradi ya kuragibisha, kutoa elimu na kusaidia watoto wa kike kukabiliana na mila potofu za ukeketaji.
Kazi ambazo zimefanywa na wanamtandao ni pamoja na mafunzo kwa wazee wa mila, mangariba, Jeshi la Polisi, mahakama, walimu, watoto, wazazi na jamii kwa ujumla ambayo yameleta chachu katika kukuza na kuimarisha uelewa wa kila mtu katika mapambano dhidi ya ukeketaji kwa watoto wa kike na wanawake. Umoja wa Afrika nao hauko nyuma katika kupambana na mila hii potofu, ambapo mkutano wa kimataifa wa kupinga mila potofu inayowadhalilisha watoto wa kike na wanawake. Katika kipindi cha leo cha Ukumbi wa Wanawake, tutazungumzia mila hii ya ukeketaji na madhara yake kwa mtoto wa kike na mwanamke.