Watoto wenye uzito mkubwa waendelea na vipimo Mlonganzila
2024-02-19 10:52:05| cri

Jopo la madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila linaendelea na uchunguzi wa vipimo kwa watoto wawili wenye umri wa miaka 7 na 4 wenye uzito uliopitiliza. Watoto hao walifikishwa hospitalini Februari 4, 2024 kwa ajili ya matibabu ya kupunguza uzito.

Vipimo hivyo vinavyohusisha watoto wenyewe na wazazi wao, vinaendelea kuchukuliwa huku matamanio ya mama yao ni kupata ufumbuzi wa changamoto inayowakabili ili wawe sawa na watoto wengine.

Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Mohammed Janabi alitoa nafasi ya matibabu bure kwa watoto hao kupitia kliniki ya uchunguzi na matibabu ya ugonjwa unaosababishwa na wingi wa mafuta kwenye damu.

Watoto hao walifikishwa hospitali kutokea nyumbani kwao Kata ya Makole jijini Dodoma na baada ya vipimo walikutwa na uzito wa kilo 76 na kilo 62 mtawalia.