Waziri wa Mambo ya Nje wa China asisitiza maelewano na kusaidiana na Ujerumani
2024-02-19 10:23:44| CRI

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema China inapenda kushirikiana na Ujerumani ili kuelewana na kusaidiana, kuzidi kuaminiana, kuimarisha ushirikiano, na kuleta utulivu na uhakika zaidi duniani.

Bw Wang, aliyasema hayo Jumamosi alipokutana na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kando ya Mkutano wa Usalama wa Munich wa mwaka huu. Katika mkutano wao, Wang aliwasilisha salamu za dhati kutoka kwa viongozi wa China na kupongeza Mkutano wa Usalama wa Munich kwa kuadhimisha miaka 60 ambapo leo limekuwa jukwaa la kimataifa la sera za usalama lenye ushawishi duniani.

Akibainisha kwamba hali ya sasa ya kimataifa inakumbwa na shida za mara kwa mara huku yakitokea masuala makubwa na uchumi wa dunia unaodorora, Wang alisisitiza kuwa China, nchi kubwa inayowajibika, inachukua hatua madhubuti kama nguvu ya utulivu katika dunia hii yenye msukosuko.

Kwa upande wake Scholz alimtaka Wang kufikisha salamu zake za dhati kwa viongozi wa China na kusema kuwa Ujerumani iko tayari kujiandaa kwa mawasiliano ya hali ya juu na China mwaka huu na kuhimiza mafanikio makubwa zaidi.

Pia katika siku hiyohiyo ya Jumamosi, Wang alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock na Waziri-Rais wa Bavaria Markus Soeder, miongoni mwa wengine.