Waziri wa mambo ya nje wa China alaani uongo unaohusiana na Xinjiang
2024-02-19 10:34:18| CRI

Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi amelaani uongo juu ya mauaji ya kimbari na watu kufanyishwa kazi kwa nguvu huko Xinjiang.

Akijibu maswali baada ya kutoa hotuba muhimu kwenye Mkutano wa Usalama wa Munich, Bw. Wang alisema baadhi ya nguvu za kisiasa zimeeneza uongo mwingi unaohusiana na Xinjiang na kutengeneza habari feki nyingi kote duniani. Amesisitiza kuwa hayo yanayoitwa “mauaji ya kimbari” ni uongo mtupu.

Alibainisha kuwa tangu Mkoa Unaojiendesha wa Kabila la Wauigur wa Xinjiang ulipoasisiwa, idadi ya watu wa Kabila la Wauigur kwa sasa imeongezeka kutoka zaidi ya milioni tatu hadi zaidi ya milioni 12. Wastani wa umri wa kuishi wa watu wa makabila mbalimbali ya Xinjiang umeongezeka kutoka miaka 30 hadi miaka 75.6. Huo ndiyo uthibitisho mzuri zaidi juu ya kulinda haki za binadamu. Kuhusu suala la Wauigur kufanyishwa kazi kwa nguvu, Wang alisema shutuma kama hizo zinatolewa na wale wanaotaka kuwakashifu wengine.

Alisema maendeleo ya kasi ya China yanazifanya baadhi ya nchi ziwe na wasiwasi, hivyo zinatunga uongo kuhusu Xinjiang ili kuzuia maendeleo ya China. Hata hivyo alisema China pia ina haki ya kupata maendeleo, akibainisha kuwa soko kubwa la China litazipatia nchi mbalimbali fursa mpya ya maendeleo na ustawi wa pamoja kote duniani.